Jumanne 9 Juni 2026 - 11:41
Mwimbaji Mmarekani awasilisha shairi la kiirfani la Imam Khomeini katika sherehe za Ghadir huko Jakarta

Hawza/ Sambamba na kufanyika hafla ya kumbukumbu ya miaka thelathini na saba ya kufariki kwa Mtukufu Imam Khomeini (ra) pamoja na sherehe kubwa ya Idi Tukufu ya Ghadir Khum huko Jakarta, Mustafa Debu, mwimbaji maarufu wa Kimarekani–Indonesia, alipokelewa kwa mapokezi makubwa na waliohudhuria baada ya kuwasilisha kazi mbalimbali za kuwasifu Ahlul-Bayt (as) pamoja na shairi la kiirfani la Imam Khomeini (ra).

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza akinukuu Idara ya Mahusiano ya Umma ya Mshauri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, programu hii ya kitamaduni na kisanaa ilifanyika kwa ushiriki wa Wairani wanaoishi nchini humo, shakhsia za kitamaduni, Waislamu wa Indonesia na wapenda utamaduni pamoja na maarifa ya Kiislamu katika ukumbi wa Ofisi ya Ushauri wa Utamaduni na Husseiniyya ya Imam Khomeini (ra) mjini Jakarta.

Katika hafla hiyo, Mustafa Debu aliwasilisha kazi maarufu ya kiroho, pamoja na kusoma mashairi kuhusu fadhila za Ahlul-Bayt (as), jambo lililozalisha mazingira ya kiroho na ya hamasa kubwa kwa washiriki.

Aidha, aliwasilisha shairi maarufu la kiirfani la Imam Khomeini (ra), shairi hilo likiwa ni miongoni mwa mashairi mashuhuri ya kiirfani ya mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na lilipokelewa kwa shangwe.

Mustafa Debu, ambaye pia anajulikana kwa jina la Kumayl Mustafa Dawud, ni miongoni mwa nyuso maarufu katika muziki wa kiroho nchini Indonesia.

Yeye alizaliwa nchini Marekani na kwa miaka mingi sasa ameishi na kufanya shughuli za kisanaa nchini Indonesia, Debu amepata umaarufu wa kimataifa kama mwimbaji mkuu wa kundi la muziki la Debu, kundi ambalo kupitia mchanganyiko wa muziki wa jadi, wa kiirfani na wa kiroho limefanya maonesho mengi katika nchi mbalimbali za Kiislamu na zisizo za Kiislamu, na kuvutia hadhira kubwa.

Kazi za msanii huyo zimejengwa zaidi juu ya dhana kama vile mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hali ya kiroho, amani, maadili na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as), na kwa sababu hiyo amepata umaarufu mkubwa miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii nchini Indonesia.

Debu kabla ya kuwasilisha shairi la Imam Khomeini (ra), katika maelezo mafupi aligusia nafasi ya kiroho na athari ya kimataifa ya mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisema kuwa; kuwasilisha kazi hiyo ni namna ya kutoa heshima kwa shakhsia na urithi wake wa fikra na irfani.

Alisisitiza: "Mashairi ya Imam Khomeini (ra) yamejaa maudhui ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu, irfani na hali ya kiroho, na yana uwezo wa kuathiri hadhira mbalimbali bila kujali mipaka ya lugha au utaifa."

Programu hii iliandaliwa kwa juhudi za Ofisi ya Ushauri wa Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, ambapo washiriki pamoja na kuadhimisha kumbukumbu ya Imam Khomeini (ra), pia walisherehekea Idi kubwa ya Ghadir Khum.

Hotuba, maonesho ya programu za kitamaduni na kisanaa, qaswida za kuwasifu Ahlul-Bayt, pamoja na ufafanuzi wa vipengele vya shakhsia na fikra za Imam Khomeini (ra), vilikuwa miongoni mwa sehemu nyingine za hafla hiyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha